Mlimbwende wa taji la urembo katika gereza kuu la wanawake la Lang'ata (Miss Lang’ata Prison 2016) Jijini Nairobi amehukumiwa kifo baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mpenzi wake aliyefamika kwa jina la Farid Mohamed mwaka 2015.
Mrembo huyo mwenye jina la Ruth Wanjiku Kamande amepatikana na kosa la kumuua mpenzi wake huyo katika mtaa wa Buruburu, Nairobi mnamo tarehe 20 Septemba, 2015 baada ya kuwa na mvutano kati yao.
Jaji Jessie Lessit amesema upande wa mashtaka ulithibitisha kumkuta mshatikiwa na hatia pasipo kuwa na shaka yoyote ambapo amedai kwamba vitendo vya Kamande vilionyesha aliua kwa kukusudia.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari kutoka Kenya vimeripoti kwamba mrembo huyo alijitetea kwamba mzozo kati yake na mpenzi wake ulikuja pale alipoiona kadi ya hospitali iliyoashiria kwamba Mohammed alikuwa akipokea matibabu ya Ukimwi.
Aidha ameeleza kwamba mpenzi wake huyo (marehemu Mohamed) alimwambia wakati huo ni heri wafe wote kuliko hali yake ya Ukimwi ifahamike hadharani ambapo wakati mzozo ukiendelea ulimpelekea kumchoma na kisu kilichokuwa kinachotumiwa jikoni.
Pamoja na hayo mahakama imekataa utetezi wa Bi Wanjiku wa kwamba marehemu alijaribu kumbaka ambapo ilielezwa kuwa uchunguzi wa madaktari ulionyesha hakukuwa na ukweli kuhusu madai hayo.
Wanjiku kwa sasa ambaye ana umri wa miaka 25 wakati anakamatwa ndiyo alikuwa amejiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kusomea masuala ya biashara, kwa mujibu wa wakili wake.
Wanjiku amekuwa mahabusu tangu mwaka 2015 katika gereza la Lang'ata akisubiri maamuzi ya mahakama dhidi ya shtaka lake.
0 Comments