Sheria Mpya Kudhibiti Uzito wa Magari Kuanza Mwakani

Sheria Mpya Kudhibiti Uzito wa Magari Kuanza Mwakani


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, ameitaka kurugenzi ya Usalama na Mazingira katika wizara hiyo kutoa elimu kuhusu kuanza kutumika kwa sheria mpya ya udhibiti wa uzito wa magari ya jumuiya ya afrika ya Mashariki ya mwaka 2016.


Akizungumza jijini Dodoma Mhandisi Nyamhanga, amesema sheria hiyo mpya ya udhibiti wa uzito wa magari itaanza kutumia Januari Mosi, mwakani.


“Hakikisheni wadau wote wa usafirishaji hapa nchini wanapata uelewa wa kutosha kuhusu sheria mpya ya udhibiti wa uzito wa magari itakayotumika katika nchi zote za Afrika Mashariki ili kuwawezesha kudhibiti athari za uharibifu wa barabara na kuepuka adhabu zilizomo katika sheria hiyo” amesema Mhandisi Nyamhanga.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu, amesema Wizara yake itashirikiana kikamilifu na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika kuhakikisha sheria hiyo mpya inatekelezeka kwa maslahi ya wasafirishaji na miundombinu ya barabara.


Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira wa Wizara hiyo, Mhandisi Julius Chambo, amesema idara yake imejipanga kutoa elimu kwa wadau wote ili wafahamu sheria hiyo, fursa zake na adhabu zilizomo kwa watakaozidisha uzito na kuharibu barabara.


Amewataka wadau wote wa usafirishaji na watumishi katika mizani zote nchini kuielewa sheria hiyo, kuifanyia kazi na kuwa waadilifu ili kulinda miundombinu ya barabara hapa nchini na kuepuka adhabu za faini na vifungo zilizomo katika sheria hiyo.


Mkutano wa siku moja wa wadau wa usafirishaji nchini ni sehemu ya mkakati wa Serikali kujenga uelewa wa pamoja kati yake na wadau wa usafirishaji katika kuelewa sheria hiyo na kuifanyia kazi.

Post a Comment

0 Comments