CAG aponda tochi trafiki

CAG aponda tochi trafiki


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, amekosoa mfumo wa kielektroniki wa tochi za usalama barabarani, huku akishauri kuimarishwa ili kuwa na matokeo sahihi.

Alitoa kauli hiyo juzi jioni alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kurejea nchini akitoa New York, Marekani, kuhudhuria mkutano wa kwanza wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) na Kikao cha 72 cha Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa (UNBoA).

Alisema wamebaini uwekezaji katika mifumo ya kielektroniki umewezesha kupata matokeo sahihi na kuzuia upotevu wa mapato.

Akitoa mfano katika ujenzi wa taasisi imara, CAG Assad alisema Tanzania inatumia toshi za kukamata wanaofanya makosa barabarani, lakini akakosoa utekelezaji wa mradi huo akieleza kuwa unaongozwa na binadamu ambaye hakuna mfumo wa kumwongoza pale anapowasha kwa ajili ya kukamata aliyetenda kosa.

"Tunataka tochi ikiwashwa tupate majibu moja kwa moja kupitia mfumo kuwa ilipowashwa, dereva alikuwa amevunja sheria -- kuwa ametembea mwendo usitotakiwa kwenye eneo fulani ikisoma moja kwa moja kwenye mfumo," alisema na kuongeza:

"Tunataka tuwe na mifumo ya 'ku-control' (kumdhibiti) anayeshika tochi na siyo yeye kuamua ili mwisho wa siku tupate majibu sahihi yenye kuridhisha na hili litawezekana iwapo tutakuwa na mfumo uliofungwa moja kwa moja."

Kwa mujibu wa CAG, kukiwa na mfumo sahihi, maana yake hakutahitaji hadi waziri kuingilia kati ili mambo yawe sawa.

CAG Assad pia aliwajibu waandishi wa habari waliotaka ufafanuzi zaidi juu ya kauli yake aliyoitoa kuwa nchi nyingi hazina taasisi zenye nguvu bali watu wenye nguvu.

Akiwa Marekani, CAG alihojiwa na Kituo cha Runinga cha UN na kutoa kauli hiyo ambayo aliisisitiza tena kwenye mkutano wake na wanahabari juzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Prof. Assad alisema lengo namba 16 la SDG linazungumzia kuzingatia amani na kufanya taasisi imara zenye nguvu na kwamba ni ngumu kulitekeleza hasa kwa upande wa nchi kuwa na mifumo imara na thabiti itakayofanya taasisi ziwe imara kuliko viongozi wanaosimamia.

"Katika miaka michache iliyopita baadhi ya nchi zimekuwa na viongozi wenye nguvu kuliko taasisi. Sisemi si muhimu kuwa na viongozi wazuri na imara la hasha," alisema na kuongeza:

"Ninachosisitiza kuwa ni muhimu zaidi kuwa na mifumo imara itakayozifanya taasisi kuwa bora na zenye nguvu, ili kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kwa kuzingatia weledi, kanuni na sheria.

"Iwapo nchi ina taasisi imara hata kama kiongozi wake si wazuri sana, mifumo thabiti yenye nguvu itasimamia maslahi ya umma na kuweza kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza. "Tatizo la nchi nyingi wanateuwa watu wazuri sana watakaosimamia taasisi.

Bila uwapo wa mifumo imara, thabiti au madhubuti haitasaidia."

Post a Comment

0 Comments