Mastaa wamimina maneno ya pongezi kwa Jokate

Mastaa wamimina maneno ya pongezi kwa Jokate


BAADA ya wikiendi iliyopita nyota njema kumuwakia mwanamitindo na msanii maarufu nchini Jokate Mwegelo kutokana na Rais Dk John Pombe Magufuli kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, mastaa mbalimbali wameibuka na kutoa neno juu ya nafasi aliyopata mrembo huyo. Mastaa wengi wameonekana kufurahia uteuzi huo ambapo baadhi yao waliamua kutoa yao ya moyoni huku wakimpongeza kama yanavyosomeka hapa chini;

ILLUMINATA POSHI ‘DOTNATA’
Jokate nafasi aliyopewa ataiweza vizuri kwa sababu alishakuwa kiongozi wa vijana CCM namuombea Mungu amsaidie sana najua atakutana na changamoto nyingi kwa kuwa hakuzoea kuletewa kesi na watu wazima, lakini kwa sababu ni msomi na muelewa atafanya kazi vizuri sana ili aweze kumwakilisha vyema rais wetu aliyemteua.

Tunajua wanawake wengi kwa sasa tunaweza zaidi kwa kujiamini siyo mambo ya kizamani. Nawaomba Watanzania wamwangalie kwa jicho la sasa ya nyuma waache. Kila mtu ana rekodi ya maisha yake, hii ni bahati kubwa sana kwa binti mdogo kama huyu kuwa mkuu wa wilaya.

Mungu alishamchagua kuwa kiongozi. Kikubwa wanawake wote tumpongeze binti yetu na dada walio sawa naye kwa umri wamsapoti na wafuate nyayo zake. Hakuibuka tu kuwa kiongozi bali amesukwa kwanza na mkuu wa nchi akaona anafaa.

JIMMY MAFUFU
Ni baraka kwetu kama tasnia na haya ni maombi, sisi waigizaji watumishi wa Mungu tumekuwa tukimsihi Mungu kutuinulia wasanii miongoni mwetu watakaoingia katika nafasi za uongozi, kitu kizuri ni kwamba Jokate ni mtu makini hivyo hatutegemei aibu kutoka kwake.

SALMA JABU ‘NISHA’
Ni kitu kizuri nampongeza Rais Magufuli na wasaidizi wake na Jokate Mwegelo pia, anastahili sana ukuu wa wilaya ana sifa zote na Mwenyezi Mungu amjaalie aje afike mbali zaidi.

FAIZA ALLY
Anastahili na nimefurahi sana nimependa maamuzi ya rais pia kama mwanamke najivunia sana kuona mwanamke mwenzangu mwenye cheo na madaraka ya juu.

TUNDA SEBASTIAN
Kwanza kabisa nampongeza sana ni hatua kubwa ambayo kila mwenye akili timamu lazima asikie wivu!

ISABELA MPANDA
Mimi nimefurahi sana pia kujiheshimu kwake kumemfanya rais amteue.

ZENA ABDALLAH ‘JIKE SHUPA’
Nimependa maana Jokate hana mambo ya mjini, mambo yake ni kimyakimya yaani kwa sasa huwezi kumjua mpenzi wake siyo kama sisi wakina Jike Shupa ukimpata mpenzi mpya dunia nzima itajua, nampongeza sana Jokate kwa kweli.


MAHSEIN AWADH ‘DK. CHENI’
Nimefarijika sana tena sana Jokate kupata ukuu wa wilaya. Rais Magufuli ameamua kutupa nafasi vijana na hatutamuangusha.

ISABELA FRANCIS ‘VAI WA UKWELI’
Mungu ambariki Jokate na namshauri afanye kazi vizuri pia abadilike kidogo maana ameshakuwa kiongozi sasa siyo kama alivyokuwa zamani.

KULWA KIKUMBA ‘DUDE’
Ni jambo jema, kwanza Jokate ni mtu ambaye amejishirikisha sana katika mambo ya kijamii, ukiachana na kuwa kijana machachari wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pia amekuwa akijihusisha na mambo yanayohusu vijana, ni mbunifu pia hivyo ana haki ya kuwa kiongozi kwa sababu amezaliwa kama kiongozi kwani kuna vitu amevifanya ambavyo hakuna mtu mwingine amewahi kuvifanya, kifupi ni msichana anayejielewa, atakuwa ni mmoja kati ya viongozi bora kabisa naamini atafika mbali, nimefurahi sana.

SAUDA MWILIMA
Kwa kweli ni jambo la kupongezwa sana kwa hatua hiyo maana ameonyesha mfano mzuri kwa vijana kwa juhudi zake za upambanaji wa kazi na kujitoa kwa jamii pia kujijengea heshima katika jamii.

MARY MAWIGI
Nampongeza sana Jokate, juhudi na malengo yake yamempa heshima ya kufika hapo alipo, namtakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yake pia tunamshukuru rais wetu kwa kuamini katika tasnia.

Post a Comment

0 Comments