Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuna asilimia kubwa ya watu wanaoumwa ugonjwa wa vidonda vya tumbo, wanaweza kuwasababishia wapenzi wao ugonjwa huo endapo watakuwa wanafikiria sana juu ya ugonjwa huo anaoumwa mpenzi wake.
Hayo yamebainishwa na Afisa Mipango katika mradi wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele kitaifa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Oscar Kaitaba wakati alipokuwa anazungumza na www.eatv.tv na kusema, chanzo cha ugonjwa huo ni 'acid' nyingi inayozalishwa kutoka kwenye mwiili wa binadamu, baada ya kuwepo na hasira, mawazo pamoja na ukosefu wa mlo kamili.
"Vidonda vya tumbo haviambukizi kama watu wanavyosema huko mitaani, ila mtu anaweza kupata vidonda hivyo ikiwa yupo na mpenzi wake, mume au mke halafu akawa na mawazo ya kumfikiria kama atapona au atakufa, na kusababisha na yeye kuumwa ugonjwa huo kutokana na mawazo aliyokuwa nayo pamoja na kushindwa kula vizuri lakini sio kwamba inaambukiza moja kwa moja", amesema Dkt. Kaitaba.
Pamoja na hayo, Dkt. Kaitaba ameendelea kwa kusema "muda mwingine sababu za kiuchumi, mawazo na hasira huwa inasababisha kutengeneza 'acid', na 'acid' ikiwa nyingi mwilini ndipo inapochimba utumbo na kupelekea mtu kujikuta katika ugonjwa wa vidonda vya tumbo. Vidonda vya tumbo vinatibika kabisa ila cha msingi mgonjwa anapaswa kwanza kukutana na wataalamu wa afya kabla ya kuanza kutumia dawa ya aina yoyote".
Dkt. Oscar Kaitaba ameeleza hayo baada ya kuwepo tetesi kwenye jamii ya kitanzania kuwa ugonjwa wa vidonda vya tumbo huweza kumuambukiza mtu kwa kutumia vitu ambavyo mgonjwa anavitumia kama kikombe na vitu vingine.
Msikilize hapa chini Dkt. Oscar Kaitaba akielezea zaidi juu ya ugonjwa huo na tiba yake
0 Comments