NaneNane Simiyu: Naibu Waziri Wa Kilimo Atao Wito Kwa Wakulima Kutumia Zana Bora Za Kilimo, Kulima Kilimo Chenye Tija

NaneNane Simiyu: Naibu Waziri Wa Kilimo Atao Wito Kwa Wakulima Kutumia Zana Bora Za Kilimo, Kulima Kilimo Chenye Tija



Na Stella Kalinga, Simiyu
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt. Mwanjelwa ametoa wito kwa wakulima kote nchini kulima kilimo chenye tija kwa kutumia zana bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kupata mavuno mengi na bora.


Dkt. Mwanjelwa ameyasema hayo Agosti Mosi, mara baada ya kukagua mabanda ya maonesho ya Kilimo katika Uwanja wa Nanenane wa Kanda ya Ziwa Mashariki uliopo Nyakabindi Bariadi, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu.


Dkt. Mwanjelwa amesema Serikali kupitia Mfuko wa pembejeo unatoa mkopo wa pembejeo kwa riba ndogo sana, hivyo akatoa wito kwa wakulima wote nchini kwenda katika Halmashuri zao na kupata utaratibu wa kuomba mikopo hiyo ili waweze kupata mikopo itakayowawezesha kununua zana bora za kilimo.


“ Nitoe wito kwa wakulima wote nchini wajitahidi sana kwenda kwenye kulima kilimo cha kisasa kilimo chenye tija, sisi kama Serikali tuna mfuko wetu wa pembejeo unaotoa mikopo kwa riba ndogo sana, hivyo wakulima wanaweza kuomba mikopo hiyo na kwenda kununua pembejeo bora za Kilimo” alisema Dkt. Mwanjelwa.


Katika hatua nyingine Dkt. Mwanjelwa amewataka maafisa ugani kuwafuata wakulima shambani badala ya kukaa ofisini, ili kuwapa elimu ya kilimo bora na kuwawezesha wakulima kufikia lengo la kulima kilimo chenye tija.


Naye Baraka Itemu mkulima wa Mpunga kutoka Geita ametoa wito kwa wakulima wenzake kote nchini kuachana na matumizi ya jembe la mkono na jembe la kukokotwa na ng’ombe kwa kuwa ni teknolojia iliyopitwa na wakati na haina tija katika uzalishaji.


“ Mimi ni mkulima wa mpunga binafsi matrekta yamenisaidia sana maana naweza kulima eneo kubwa kwa muda mfupi na nikapata mazao mengi, natoa wito kwa wenzangu wanaotumia majembe ya mkono na ya kukokotwa na ng’ombe waache waende kwenye makampuni ya matrekta wakakope, ili waweze kuzalisha mazao kwa wingi” alisema Baraka.


Nao wauzaji wa zana bora za kilimo waliofika katika maonesho ya Nanenane Bariadi mkoani Simiyu wamesema wako tayari kushirikiana na wakulima ili kuhakikisha wanapata zana hizo, huku wakibainisha kuwa wakulima wasiokuwa na uwezo wa kununua zana hizo kwa fedha taslimu wako tayari kuwakopesha.


Maonesho ya Nananane mwaka 2018 yanafanyika Kitaifa Mkoani Simiyu, ambapo yameanza leo na yatahitimishwa Agosti 08, 2018.

Post a Comment

0 Comments