WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora, SSP Ally Mkalipa awakamate watu wote waliohusika katika ubadhifu uliofanyika kwenye mradi wa mashine ya kukobolea mpunga ya kijiji cha Chomachankola, wilayani Igunga.
Imeelezwa kuwa halmashauri ya wilaya ya Igunga ilitoa sh. milioni 35 kwa ajili ya kukiwezesha kijiji cha Chomachankola kununua mashine ya kukoboa mpunga lengo likiwa ni kuwawezesha wakulima kuliongezea thamani zao hilo kwa kukoboa mpunga na kuuza mchele.
Alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Agosti 16, 2018) baada ya Mbunge wa jimbo la Manonga, Seif Gulamali kumlalamikia kuhusu fedha zilizotolewa kwa ajili mradi wa mashine ya kukoboa mpunga ya kijiji hicho, ambazo zilitolewa miaka mitano iliyopita hadi sasa mradi haujaanza.
Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Igunga kuhakikisha watu wote waliohusika na ubadhilifu huo ambao ni Katibu wa kamati ya mradi huo Daudi Mwangaluka, John Fumbuka (Mjumbe, Yusta Thomas (mweka hazina) na Hansa (mkandarasi) wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Alisema Serikali haiwezi kukubali kuona fedha za wananchi zilizotolea kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikitafunwa na watu wachache wasiokuwa waaminifu, ambao wanakwamisha ukuaji wa uchumi wa kijiji.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekemea vitendo vya watoto wa kike kukatishwa masomo kwa kupewa ujauzito, ambapo amewata wazazi na walezi wilayani hapa hawakikishe wanasimamia elimu ya mtoto wa kike ili aweze kumaliza masomo yake.
Waziri Mkuu alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii kwa kuachwa waendelee na masomo yao bila ya usumbufu wa aina yoyote na atakayebainika kukatisha masomo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Alisema kila mkazi wa wilaya hiyo hususani vijana wawe walinzi wa watoto wa kike na ni maruku kuoa mwanafunzi au hata kumuweka kinyumba kwa kuwa ni kinyume na sheria na atakayebainika Serikali imeweka dhabu kali ambayo ni kifungo kisichopungua miaka 30 gerezani.
“Hapa wanafunzi wengi wanashindwa kuendelea na masomo yao kwa ajili ya kupewa ujauzito, sasa kabla ya kutenda jambo hilo ni lazima ujifikirie maana adhabu yake ni kubwa. Ukimpa ujauzito mwanafunzi au kumuoa jela miaka 30, ni bora ukaachana kabisa na wanafunzi,”.
Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi wote kusoma kwa bidii na wahakikishe wanafika hadi chuo kikuu ili watimize ndoto zao walizojiwekea maishani na kamwe wasikubali kushawishika kwa sababu watashindwa kufikia lengo waliyojiwekea.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 17, 2018.
0 Comments