WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema baada ya mitatu Serikali itakuwa imefikia asilimia 90 ya lengo iliyojiwekea la kukuza uchumi kutoka wa chini hadi wa kati kwa kupitia sekta ya viwanda.
Amesema Serikali imedhamiria kukuza uchumi waTaifa na wa wananchi ili kufikia wa kati ifikapo 2025, hivyo amewaomba wananchi waendelee kuipa ushirikiano.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Agosti 16, 2018) alipozungumza na wananchi katika kijiji cha Chomachankola wilayani Igunga akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Igunga, Tabora.
“Tunaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waipe ushirikiano Serikali yao katika kipindi hiki ambacho inaendelea kutekeleza ahadi yake ya kuinua uchumi,” alisema.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli pamoja na zile zilizomo kwenye Ilani ya uchaguzi.
Waziri Mkuu alitaja ahadi hizo kuwa ni pamoja na ujenzi na ufufuaji wa viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali nchini, kikiwemo kiwanda cha kuchambua pamba cha Manonga.
Alisema kiwanda cha kuchambua pamba cha Manonga ambacho kisimama kuchambua pamba kwa miaka 25 na sasa kimefufuliwa na kinafanya kazi, hivyo aliwaomba wananchi watoe ushirikiano kwa mwekezaji.
Wakati huo huo, wananchi wa wilaya ya Igunga waliishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais, Dkt Magufuli kwa kuwezesha kukufuka kwa kiwanda chao cha kuchambua pamba cha Manonga.
Akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya wananchi, Mbunge wa jimbo la Manonga, Seif Gulamali alisema ufufuaji wa kiwanda hiko umeongeza tija kwa wakulima wa zao la pamba na wananchi kwa ujumla.
Alisema mbali na kufufuliwa kwa kiwanda hicho, pia wanaishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali za kuboresha maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kupeleka sh. milioni 500 za ujenzi wa daraja la Mto Manonga.
“Umbali wa kutoka Manonga hadi Shinyanga ni kilomita 40, lakini tunalazimika kwenda hadi Nzega ili kufika Shinyanga ambako ni zaidi ya kilomita 130, tunaishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa daraja hilo kwa kuwa litaturahisishia safari,” alisema.
Mbunge huyo aliongeza kuwa miradi mingine mingine inayotekelezwa Serikali inayotekelezwa katika jimbo la Manonga ni pamoja na ujenzi wa mabweni kwenye shule tatu za sekondari na ujenzi wa kituo cha afya cha Simbo ambayo gharama yake inakadiriwa kuwa sh. milioni 880.
Kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano huo wa hadhara, Waziri Mkuu alitembelea na kukagua ufungaji wa mitambo mipya na shughuli ya kuchambua pamba katika kiwanda cha kuchambua pamba cha Manonga, ambapo amisema amefurahishwa na kazi inayoendelea kiwandani hapo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 17, 2018.
0 Comments