Wenye matatu kuchota ujuzi Dart

Wenye matatu kuchota ujuzi Dart


Dar es Salaam. Wafanyabiashara wamiliki wa matatu nchini Kenya wamefanya ziara nchini ili kupata uzoefu wa namna Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ulivyowashirikisha wamiliki wa daladala nchini.


Ujumbe wa wafanyabiashara 10 umeanza ziara ya siku mbili leo Agosti 30 na wamepokewa na uongozi wa Wakala wa Serikali wa Dart.


Katibu wa umoja wa wamiliki wa matatu, Githaiga Weri amesema ziara yao inalenga kukuza uelewa kwa kuwa Kenya inatarajia kutekeleza mradi kama huo miaka michache ijayo.


"Tunatarajia kuwa na mradi kama huu mwaka 2022 lakini Serikali imeshaanza mchakato wa awali, ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau ndiyo maana tumekuja kuona wenzetu walishirikishwa vipi na wananufaikaje ili nasi tuweze kufanya vizuri," amesema Weri.


Amesema mradi wa Dart ni miongoni mwa iliyo muhimu na mizuri inayoweza kutumika kutatua changamoto za usafiri katika Jiji la Nairobi na kupunguza msongamano wa magari.


Kaimu Mkurugenzi wa Dart, Mhandisi Ronald Lwakatare amesema la muhimu ni kutoa elimu kwa wananchi, madereva na wafanyabiashara wengine wadogo ili waujue vizuri mradi huo kwa kuwa wasipofanya hivyo watapata changamoto nyingi.


"Wamiliki wa daladala walikuwa miongoni mwa wadau muhimu na tuliwashirikisha kwa kuwataka kuunda kampuni ili nao wanunue magari yanayoendana na matakwa ya mradi na kuwa na namna nzuri ya kukusanya mapato," anasema Lwakatare.


Amesema shughuli ya kuwahamisha wamiliki wa gari mojamoja ilifanikiwa kwa kuwabadilishia safari na kuwapatia fedha kidogo za usumbufu, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) ikisitisha kuwaongeza muda wa leseni wamiliki wa magari ambayo mradi wa Dart unapita.

Post a Comment

0 Comments