Diwani aliyeshambuliwa atoka ICU

Diwani aliyeshambuliwa atoka ICU


Karagwe. Diwani wa Nyakahanga, Charles Bechumila aliyekuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) amehamishiwa wodi ya kawaida baada ya hali yake kiafya kuanza kuimarika.


Bechumila alijeruhiwa kwa mshale jana Agosti 29 baada ya msafara wa mkuu wa wilaya ya Karagwe mkoani Kagera kushambuliwa. 


Katibu wa Afya wa Hospitali Teule ya Nyakahanga, Jeremiah Rugimbana amesema diwani huyo alifanyiwa upasuaji jana.


Amesema alipofikishwa hospitalini hapo alikutwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake yaliyotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.


Rugimbana amesema mgonjwa huyo alikuwa na jeraha kwapani, chini ya nyonga na shingoni.


Diwani wa Kanoni, Saby Rwazo aliyemtembelea Bechumila kumjulia hali leo, Agosti 30 amesema sasa anaweza kuwatambua watu na kuzungumza nao.


Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Muheluka amesema msako uliofanywa usiku kucha na polisi umewezesha kukamatwa watu 20 wanaodaiwa kuhusika kumjeruhi diwani huyo kwa mshale.


Amesema amewasiliana na majeruhi huyo kwa simu baada ya kutolewa ICU na kwamba, msako zaidi wa watuhumiwa unaendelea.


Msafara wa mkuu wa wilaya ulishambuliwa jana saa tano asubuhi wakati kiongozi huyo na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya walipowasili katika Kijiji cha Kashanda kutatua mgogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Post a Comment

0 Comments