DC Momba aamua kuwaonyesha Chadema nguvu yake

DC Momba aamua kuwaonyesha Chadema nguvu yake



Mkuu wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Jumaa Irando ameamua kutunishiana misuli na madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwa kuwaagiza watendaji wa Serikali wasifanye nao kazi.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni mwendelezo wa kutunushiana misuli baina ya vigogo hao baada ya Agosti madiwani hao kupitia kwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ally Mwafongo kutamka kuondoa ushirikiano na Irando wakidai anaingilia mipango ya halmashauri.

Mwafongo alitoa tamko hilo kwa nyakati tofauti akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani na mikutano ya hadhara iliyokuwa ikiandaliwa na Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka na katika kikao cha kamati ya fedha cha halmashauri hiyo kilichoketi Septemba 14.

Akizungumza jana ofisini kwake, Irando alisema agizo lake limeanza kutekelezwa Septemba 18 na aliwataka watendaji wote wa Serikali kuanzia ngazi ya ofisi kuu, kata na mitaa kuacha kutekeleza maagizo, uamuzi, maelekezo, ushauri au maombi mbalimbali ikiwamo posho inayotolewa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo pamoja na madiwani wake.

Pia, alisema amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji huo, Kastory Msigala kuwajulisha wananchi namna ambavyo watapata huduma katika kipindi hicho.

Mkurugenzi mtendaji huyo alikiri kupata maelekezo kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya na kuwa tayari maelekezo hayo ameyapeleka kwa watendaji walioko chini yake.

Akizungumza kwa simu jana, Mwafongo alisema bado hajapata taarifa za maandishi kuhusu tamko la mkuu wa wilaya lakini amesikia tetesi kuhusu uamuzi huo.

Hata hivyo, alipoulizwa, Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Elia Ntandu alishauri jambo hilo kumalizwa mezani badala ya kuendekeza malumbano ambayo yanaathiri maendeleo ya wananchi.

Mwananchi:

Post a Comment

0 Comments