MATUMIZI YA PAPAI KATIKA UREMBO

MATUMIZI YA PAPAI KATIKA UREMBO


TUNDA la kitropiki la papai lina vitamini C na E likiwa na siri kubwa ya urembo na hutumika kutengeneza facials za aina mbalimbali.

Papai kando na kuliwa, hufanya kazi ya kuridhisha linapotumika kutunza uso na kulainisha ngozi ya mtumiaji bila yeye kutumia 'mikorogo' ya kuacha mabaka katika ngozi.

Bidhaa zinazotengenezwa kutokana na malighafi ya papai ni pamoja na sabuni, mafuta ya mwili, tona, moisturizer, facial peels na nyingi nyinginezo

Ukitumia maski ya papai utakuwa na sura nzuri ya asili kwa kuwa hufanya uwe na mwonekano mzuri.

Maski hii ya uso inaweza kutumika na watu wenye umri na aina yoyote kwa kuwa huwa haina madhara.

Pia inasaidia ngozi ambayo imeanza kupata makunyanzi umri unapokuwa umesonga. Kando na kupunguza makunyanzi, huondoa chunusi pia.

Ni rahisi kutengeneza maski ya papai na ukitumia itakusaidia katika kukabiliana na ngozi iliyoanza kuchoka na kung’arisha ngozi .Kuna baadhi ya njia nzuri za kuhakikisha kuwa, tunakuwa na nyuso nzuri zenye kupendeza na kuvutia ikiwemo kutumia vitu vya asili pamoja na matunda
ya aina mbalimbali ambayo husaidia zaidi katika kuimarisha ngozi.

Maski ya mchanganyiko wa papai na yai ni nzuri katika kuhakikisha kuwa unakuwa na ngozi nzuri na nyororo. Katika makala ya faida za yai tuliita maski hii 'barakoa'.

Njia hii pia husaidia hata wale wenye nyuso zinazosumbuliwa na chunusi mara kwa mara za kufanya ngozi kuwa kavu.

Unaweza kutengeneza aina hii ya maski kwa kufanya jinsi ifuatavyo:

Chukua papai ulikate kisha toa mbegu; yaani kokwa zake na ulisage kwa kutumia blenda au kupondaponda kwenye kibakuli kwa kutumia mchi.
Kisha weka mchanganyiko huo kwenye bakuli. Vunja yai na ukoroge kuhakikisha kuwa mchanganyiko huo umechanganyika vizuri.
Safisha uso wako na uondoe uchafu wote ulioganda usoni.
Kisha paka maski usoni na unapopaka hakikisha kuwa mchanganyiko huo haugusi macho yako.
Osha uso wako baada ya dakika 15. Jifute kwa kutumia taulo safi.
Baadaye paka mafuta kwenye uso wako - yale tu ya kawaida.

Post a Comment

0 Comments