Mradi Wa Kusambaza Gesi Asilia Majumbani Wafikia Asilimia 76

Mradi Wa Kusambaza Gesi Asilia Majumbani Wafikia Asilimia 76



Meneja Mradi wa usambazaji wa gesi majumbani Dar es Saaalam, Denice Byarushengo, amesema kazi ya kusambaza mabomba ya gesi asilia kwa wananchi imekamilika kwa asilimia 76.8.


Byarushengo alisema hayo jana wakati akimueleza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC), Kapuulya Musomba kuhusu hatua ambazo mradi huo umefikia.


Byarushengo alisema mradi huo unalenga kuunganisha kiwanda cha Coca Cola Kwanza Ltd. na Kiwanda cha Mafuta cha BIDCO na wateja takribani 1000 wa majumbani.


Alisema kazi hiyo pia imekwenda sambamba na kusimika mtambo wa kupunguza mgandamizo ambao nao umekamilika kwa asilimia 97.


“Uunganishaji wa mabomba umekamilika kwa asilimia 88.6, ulazaji na ufukiaji wa mabomba umekamilika kwa asilimia 56.9.


“Viainisho sita vya bomba linapopita vimeshawekwa na ujenzi wa daraja la waenda kwa miguu umekamilika kwa asilimia 90,”alisema Byarushengo .


Alisema mradi huo utahusisha kuvuka mto Ubungo na barabara ya Ubungo Maziwa na ya Mandela, kazi ambayo hadi sasa imekwisha kukamilika.


Alisema kwa barabara ya Ubungo Maziwa kazi imekamilika kwa asilimia 50, huku kwa barabara ya Mandela kazi iko mbioni kuanza.


Alisema mradi huo utawezesha upatikanaji wa gesi asilia ya kutosha katika bomba linalotoka Ubungo kwenda Mikocheni kupitia barabara ya Sam Nujoma na kusambaza gesi kwa wateja wa majumbani katika maeneo ya Ubungo, Shekilango, Mlalakuwa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sinza na Mikocheni.


Musomba alieleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo ambao utaunganisha bomba kubwa la gesi asilia la urefu wa kilomita 7.8 na lile la Ubungo kwenda Mikocheni na uwezo wa kusafirisha gesi ya futi za ujazo milioni 7.5 kwa siku.

Post a Comment

0 Comments