ocha Stars aanza kazi kwa mtandao

ocha Stars aanza kazi kwa mtandao


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kocha mpya wa timu ya Taifa (Taifa Stars), anatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia sasa ili kuanza kibarua chake kipya, lakini likafafanua kuwa tayari ameanza kazi ya kuwafuatilia wachezaji baada ya mazungumzo kufikia pazuri.

Hata hivyo, TFF haikuwa tayari kumtangaza kocha huyo mpya ambaye anakuja nchini kurithi mikoba iliyoachwa na Mtanzania Salum Mayanga.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, alisema shirikisho liko katika hatua za mwisho za kukamilisha mchakato wa kumtangaza kocha huyo mpya wa Taifa Stars.

Kidao alisema wamefikia hatua nzuri na kocha huyo mpya na tayari ameshaanza kuwafuatilia wachezaji waliokuwapo katika kikosi cha Stars hivi karibuni kwa lengo la kuanza kuijenga timu yake.

"Mchakato wa kumpata kocha mpya unaendelea vizuri, tutamtangaza mapema Agosti [mwezi huu] na habari njema ni kuwa ameshaanza kufanya kazi za timu baada ya mazungumzo dhidi yake kufikia mahali pazuri, tutakapomaliza baadhi ya taratibu, tutamtangaza," alisema katibu huyo.

Moja ya matokeo mazuri ya Mayanga wakati anaiongoza Taifa Stars ni ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyopigwa Machi 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mayanga hakufanya vizuri na timu ya Tanzania Bara katika mashindano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika mwaka jana huko Kenya na kuishuhudia Zanzibar Heroes ikicheza fainali dhidi ya wenyeji Harambee Stars.

Hivi karibuni aliyekuwa Kocha Mkuu wa Stars na mshauri wa ufundi wa timu za vijana, Kim Poulsen, aliamua kuachia ngazi baada ya TFF kushindwa kumlipa malimbikizo ya mishahara yake.

Post a Comment

0 Comments