MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewaagiza mameneja wake wote nchini kufanya operesheni sehemu za biashara baada ya kubaini baadhi ya wafanyabiashara hawatoi risiti za kielektroniki za EFD kwa kisingizio cha mfumo.
Kamishna wa Kodi za Ndani TRA, Elijah Mwandumbya, alitoa agizo hilo jana muda mfupi baada ya kufanya ziara ya kikazi katika maduka yaliyopo katika jengo la Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Mwandumbya alitembelea maduka hayo na kubaini wafanyabiashara hao wanatumia mashine hizo na wanatoa risiti kwa wateja wao.
Akizungumza baada ya ziara hiyo Mwandumbya alisema baadhi ya wafanyabiashara hawatoi risiti kwa kisingizio cha mfumo wa TRA unasumbua kitendo ambacho siyo cha kweli.
"Nitoe angalizo kwenye hili, TRA tumethibitisha hakuna hitilafu yoyote kwenye mfumo kwa sasa na wafanyabiashara wote wanapaswa kutoa risiti kwenye mauzo yote wanayoyafanya," alisema.
Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa wafanyabiashara wote kuhakikisha wanatumia mashine ipasavyo na hakuna sababu itakayokubalika ambayo itatolewa na wao ya kutokutoa risiti za EFDs.
"Jambo lingine ambalo natoa kama maelekezo kwa mameneja wote nchini wahakikishe wanafanya operesheni ya nguvu katika biashara zote nchini ili kuhakikisha wafanyabiashara wanazo mashine kwa wanaostahili kuzitumia," alisema.
Pia alisema hakuna mfanyabiashara mwenye barua ambayo inampa sababu ya kutokutoa risiti katika biashara yake.
Akizungumzia kuhusu ziara kwenye maduka yaliyopo Mlimani City, Mwandumbya alisema ziara hiyo ni mwendelezo wa utaratibu wa kukagua duka hadi duka, biashara hadi biashara mlango hadi mlango kuhusu matumizi ya EFDs.
Alisema lengo ni kuangalia wote wanaofanya biashara wana mashine na kama wanazitumia ipasavyo.
"Wafanyabiashara katika eneo hili wana mashine na wanatoa risiti katika mauzo wanayoyafanya, lakini tumeona kwa nyakati mbalimbali wapo wengine wanadanganya kidogo, wapo ambao hawana nia njema pia hawatoi risiti katika mauzo wanayoyafanya," alisema.
0 Comments