Kikongwe wa miaka 80 awaacha watu macho kodo

Kikongwe wa miaka 80 awaacha watu macho kodo


Bibi anayetambulika kwa jina la Cecilia Wangari maarufu kama Shosh amekuwa gumzo mjini Nairobi, Kenya kutokana na kazi yake anayofanya ambayo imewashangaza watu wengi.

Kikongwe huyo mwenye umri wa miaka 80 ambaye anafanya kazi ya ufundi wa radio za magari amekuwa tofauti na wazee wengine wenye umri kama wake ambao wengi wa mekuwa wakikimbilia kulima na wengine wakikaa nyumbani wakiwa tegemezi kwa watoto wao na ndugu zao.

Bi Cecilia ameonyesha utofauti huo mkubwa ambao watu wamekuwa wakibaki kutafakari mara mbili kwa kuvunja mwiko wa wazee wenzake.

Akiongea na BBC, bibi huyo amesema kuwa amezaliwa katika mji huo wa Nairobi na alikuwa akifanya biashara zake tangu miaka ya sabini kiasi ambacho kilimpelekea kuweza kumiliki gari lake mwenyewe la abiria katika kipindi hicho.




Ameongeza kuwa aliwaajiri dereva na kondakta lakini mara nyingi walikuwa wanamlaghai kuwa gari limeharibika na alikuwa akiwapa fedha za matengenezo lakini hawafanyi kama walivyokubaliana, hapo ndipo aliamua kuanza kufanya kazi hiyo ili aweze kusimamia mwenyewe mradi wake huo.

Shosh ameendelea kwa kusema, licha ya yeye kutokuwa na kisomo chochote alianza kujifunza taratibu kuanzia1991 kukarabati na kufunga radio za magari kwa fundi mmoja mara nyingi kwa kuangalia tu jinsi kazi hiyo ilivyokuwa ikifanywa.

"Fundi aliyenifundisha aliniambia ninunue vifaa vichache tu ambavyo nilitumia kujifunzia hii kazi na tangu wakati huo nimeifanya kazi hii kwa miaka yote hii, ni kazi ninayoifurahia kwa saabu ninaipenda," amesema Bi Cecilia.




Shosh ana vijana kadhaa wanamsaidia kazi kwenye duka lake na baadhi yao ni wajukuu zake ambao anasema anataka awasaidie kujimudu kimaisha na waweze kujitegemea siku za usoni lakini wateja wengi wanaofika katika duka hilo wamekuwa wakitaka huduma kutoka kwa Bi Cecilia mwenyewe.

Mzee huyo ametoa siri ya kudumu kwa miaka mingi kwenye kazi hiyo na wateja kumpenda ni kutokana na kuwa mkweli kwenye kazi yake na kuwaheshimu wateja wote na kuhakikisha anakuwa na leseni zote zinazohitajika kwenye biashara yake ili kazi yake iweze kuendelea vizuri.




"Ni lazima nihakikishe kuwa duka langu lina leseni na hata bango lililo nje ya duka na ni lazima nililipie ili kuhakisha kuwa ninafanya biashara bila ya usumbufu wowote," amesema Shosh.

Bi Cecilia amesisitiza kuwa hana mpango wa kuachana na kazi hiyo kwa sasa hata akibarikiwa kuishi miaka 200 ataendelea kuifanya.

Post a Comment

0 Comments