Uongozi wa klabu ya Simba umetangaza rasmi kucheza na timu ya Asante Kotoko ya Ghana katika tamasha lake la Simba Day, Agosti 8 mwaka huu.
Kupitia kwa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Sunday Manara, amesema Simba itachuana na timu hiyo kongwe ambayo inashiriki Ligi Kuu Ghana kwa ajili ya kuitambulisha timu yao.
Manara amewatangaza Kotoko kucheza nao baada ya hapo awali kuenea kwa taarifa kuwa Simba imewaalika wapinzani wakubwa wa Gor Mahia FC, AFC Leopards kutoka Kenya lakini amezikanusha akisema hazikuwa na ukweli.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Ghana, Kotoko wamecheza mechi 15 wakiwa kwenye nafasi ya 4 huku wakijikusanyia alama 24 na Ashanti Gold iliyo nafasi ya kwanza ina alama 27 ikiwa imecheza michezo 15 pia.
Zikiwa zimesalia siku 7 pekee kuelekea tamasha hilo, kikosi cha Simba hivi sasa kipo katika kambi maalum ya wiki mbili nchini Uturuki ambapo kimeweka kambi katika jiji la Instanbul.
Kikosi hicho baada ya kambi yake kumalizika kitaanza safari ya kurejea nchini kuanzia tarehe 4 mwezi huu tayari kwa tamasha hilo kubwa linalofanyika kila mwaka.
0 Comments